
Wakenya bado wanasubiri kwa shauku kubwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita huku matokeo ya awali yakionesha vigogo wawili wanaopewa nafasi ya kushinda wanachuana vikali.
Hadi jana Jumapili, matokeo ya Tume ya Uchaguzi, IEBC, yalikuwa yanaonesha Naibu Rais, William Ruto, anaongoza kwa idadi ndogo ya kura dhidi ya mwanasiasa wa muda mrefu na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.
Tume ya Uchaguzi tayari imejumlisha matokeo ya asilimia 70 ya majimbo kiasi 290. Miito inaongezeka kwa Tume ya Uchaguzi kukamilisha mchakato huo na kumtangaza mshindi wa kiti cha urais.
Makundi ya Haki za Kiraia, Vyama vya Wafanyakazi na mashirika kadhaa ya kimataifa yalitoa tamko la pamoja jana Jumapili linalotoa mwito wa kuwapo utulivu wakati huu matokeo yanaendelea kutangazwa.
