
Rais Joe Biden wa Marekani ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 21 hapo jana tangu mashambulizi ya kigaidi nchini humo ya Septemba 11, 2001 kwa kuweka shada la maua kwenye jengo la wizara ya ulinzi.
Maadhimisho hayo yanafanyika baada ya mwaka mmoja tangu Biden alipohitimisha operesheni ya muda mrefu na ya gharama kubwa ya kijeshi nchini Afghanistan, ambayo Marekani na washirika wake waliianzisha katika kupambana na ugaidi.
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa John Kirby amesema hotuba ya Biden itatambua athari za mashambulizi hayo ya 2001 nchini humo na ulimwengu kwa ujumla pamoja na kuwakumbuka karibu watu 3,000 waliouawa siku hiyo, baada ya watekaji wa al-Qaeda kuzidhibiti ndege za kibiashara na kuziangusha kwenye majengo ya Kituo cha kibiashara cha Kimataifa, wizara ya ulinzi na uwanja wa ndege wa Pennysylvania.
Mkewe Biden, Jill Biden alizungumza katika uwanja wa Pennysylvania huku makamu wa rais Kamala Harris na mumewe walihudhuria maadhimisho hayo kwenye jumba la kitaifa la kumbukumbu ama National September 11th Memorial, mjini New York.
