Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla ameagiza kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Daraja la Tanganyeti lenye urefu wa mita 40, lililopo Barabara ya Arusha–Longido–Namanga kuelekea nchini Kenya.
Mradi huo unatekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya shilingi bilioni 4.6, chini ya Mkandarasi Kampuni ya Jiangx Geo Engineering.
Makalla ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Septemba 5, 2025, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Longido.
Amewataka wakandarasi kuongeza kasi ili kuhakikisha daraja hilo muhimu kwa wananchi linakamilika ifikapo Desemba 2025, na kuanza kutoa huduma.
“Barabara hii ni kiungo muhimu kwa uchumi wa nchi hizi mbili, Tanzania na Kenya. Kwa kuzingatia umuhimu wake, ujenzi lazima uendane na kasi ya mahitaji ya wananchi na wageni wanaoitumia,” alisema CPA Makalla.
Wazee wa Wilaya ya Longido wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kujenga daraja hilo katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa kikwazo hasa nyakati za mvua, kutokana na maji kujaa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mzee Michael Lekule Laizer, amepongeza jitihada hizo akibainisha kuwa, mbali na shilingi bilioni 4.6 zilizotolewa kwa ajili ya daraja hilo, Rais Samia pia ametoa fedha nyingi zilizotekeleza miradi mikubwa ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara mkoani Arusha
