
Rais Samia Suluhu Hassan, amesema ulegelege wa Jeshi la Polisi nchini unatokana na upungufu wa mafunzo ndani ya Jeshi hilo.
Ameyasema hayo jana Jumanne Agosti 30, 2022 wakati akifungua kikao kazi cha maofisa wakuu waandamizi wa Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Polisi na vikosi, kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Polisi Tanzania (TPS), mkoani Kilimanjaro.
Rais Samia amesema tathimini inaonesha upungufu wa mafunzo unalifanya Jeshi la Polisi maeneo mengine liwe limelegea au kuwapo mmomonyoko wa maadili ndani yake.
Hata hivyo, amebainisha kuwa kuajiri Polisi wasio na vigezo ni sababu nyingine inayolitia aibu Jeshi hilo.
Aidha amesema baadhi ya Polisi wamekuwa wakirekodiwa mitandaoni wakifanya mambo yanayolifedhehesha Jeshi hilo kutokana na ukosefu wa maadili.
Amewataka kuzingatia maadili ya kazi hilo ili kuinua heshima yake iliyoanza kutoweka miongoni mwa wanajamii.
