Ramadhani Shaban (21) maarufu “Kocha” Mkazi wa Buronge Manispaa ya Kigoma Ujiji Anashikiliwa na Polisi mkoani hapo kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwamba ametekwa wakati alijiteka yeye mwenyewe kwa msaada wa Rafiki zake ili kuwezesha Wazazi wake kutoa fedha kwa Watekaji feki aweze kukombolewa na kuwa huru.
Akizungumza na Wanahabari leo September 04,2024 Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, Filemon Makungu amesema May 14,2024 Shabani alitoa taarifa kwa Wazazi wake akidai ametekwa na Watekaji wanadai Tsh. milioni 2.5 ili waweze kumuachia.
Akiwa mafichoni ambapo alikuwa amejificha Mtu huyo alikuwa akipiga simu kwa Wazazi wake watoe fedha haraka ili waweze kumuachia kwani wakichelewa Watekaji wanaweza kumuua kabisa ambapo kufuatia shinikizo hilo Wazazi wa Mtu huyo walitoa taarifa Polisi ambapo upelelezi ulianza mara moja huku Polisi wakiwasihi Wazazi kutotuma fedha kwa Mtu yeyote kuhusiana na tukio.
“Wakati Polisi wakiendelea na upelelezi Ramadhani alifikishwa na Wazazi wake Kituo cha Polisi Mkoa Kigoma wakieleza kuwa amepatikana eneo la Msimba Dampo nje kidogo ya Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kutoa fedha kwa Watekaji.
Hata hivyo polisi waligundua kuwa Mtuhumiwa huyo akiwa na Washirika wake wawili Kassimu Kibona na Ramadhani Issa walitoa taarifa za uongo zilizoleta hofu na tahatuki ndani ya jamii kwa nia ya kujipatia fedha na hivyo kuwakamata ambapo wanatarajia kufikishwa Mahakamani upelelezi utakapokamilika.
