
Vyombo vya habari nchini Afrika Kusini vimeripoti kuwa kiongozi wa kundi linalopinga wahamiaji nchini humo Nhlanhla Lux Dlamini (33), amekamatwa.
Dlamini alikamatwa jana Alhamis na amezuiliwa katika kituo cha polisi katika mji mkuu wa kibiashara wa Johannesburg huku sababu za kukamatwa kwake hazijabainishwa.
Kundi lake la operation Dudula, limekuwa likifanya kampeni dhidi ya raia wa kigeni wasio na vibali nchini.
Uungwaji mkono wa kundi hilo umekuwa ukiongezeka miongoni mwa jamii ya Wafrika Kusini wanaohisi kutengwa.
Kuna wasiwasi kwamba kampeni zake zinaweza kusababisha kuzuka tena kwa ghasia za chuki dhidi ya wageni nchini.
