Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa nchini kusikilizwa na kueleza misimamo yao.
Prof. Kabudi amesema hayo leo, Oktoba 7, 2026, wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Katika hafla hiyo, Prof. Kabudi pia amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya siasa kuheshimiana wanapoeleza tofauti zao za kisiasa, akisisitiza kuwa matumizi ya lugha yenye ukakasi yanaweza kudhoofisha heshima katika siasa.

Amesema si sahihi kumuita kiongozi mwenzake ambaye amechaguliwa kuwa “haramu”, akieleza kuwa kuna namna nyingine ya kueleza kutoridhishwa na uhalali wa uongozi bila kutumia neno hilo.
“Huwezi kumwita mwenzako kiongozi haramu, unaweza kusema hayupo hapo kihalali. Neno haramu katika Kiswahili lina maana ya ukakasi mkubwa sana,” amesema Prof. Kabudi.
