
Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thadeus Ruwa’ichi ameongoza mamia ya waamini wa kanisa hilo jimboni humo katika Misa Takatifu ya Mavuno.
Misa hiyo iliadhimishwa Jumamosi Novemba 19, 2022 katika viwanja vya Msimbazi Centre, moja ya maeneo yanayomilikiwa na Kanisa hilo.
Akizungumza wakati akihubiri Askofu Mkuu Ruwa’ichi amewataka Wakristo kumshukuru Mungu kwa makuu anayowatendea na kwa wale ambao wanaamini huenda hawajatendewa chochote, wakumbuke kuwa hata uhai walio nao wamepewa na Mungu.
“Tumekusanyika hapa kumpa Mungu shukrani kwa yale anayotutendea katika maisha yetu, ambako kwa kushukuru anatupa baraka na neema tunazohitaji.
“Mungu anatutaka tutoe matoleo kwa ajili ya utume wa kanisa na wahitaji, ukarimu ni fadhila ya mtu wa Mungu, hatufanyi ukarimu kutokana na utajiri tulionao bali kutokana na tunayopata.
“Pia tumekusanyika hapa kumwomba Mungu atujalie baraka ya mvua, kwa sababu hatuna maji, tusikate tamaa kwa kuwa anawezesha yote tukijiungamanisha kwake,” alisema.
Hata hivyo, alionya kuwa katika maisha ya kila siku kuna baadhi ya Wakristo wanapopata mafanikio hawamshukuru Mungu badala yake huonesha majivuno.
“Baadhi ya wanadamu wanapofanikiwa huvimba kichwa,” alisema.
Askofu mkuu Ruwa’ichi aliongeza kuwa ni vema Wakristo wakaiga mfano wa mkoma aliyerudi kwa Yesu kumshukuru baada ya kuponywa Luka 17:15 huku wenzake Tisa wakienda zao.
“Sisi sote ni wakoma kutokana na udhaifu na dhambi zetu, tupaze sauti zetu kuomba huruma ya Mungu,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa maisha ni safari yenye changamoto ambapo binadamu anahitaji msaada wa Mungu katika kila jambo la msingi analolifanya.
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam lina dekania 17, parokia kamili 147 na parokia teule 15 ambazo zilishiriki Ibada hiyo ya misa takatifu.
