
Askofu David Chomba wa huduma ya Lighthouse Mission Church ya jijini Dar es Salaam, amewashauri wachungaji kujiendelea kielimu hususan wakati huu ambapo jamii kubwa imeelimika.
Askofu Chomba ambaye kitaalauma ni mwalimu, amesema wachungaji wanapaswa kutambua kuwa kizazi cha sasa ni cha kwanini hivyo elimu kwao itatasaidia kutoa majibu.
Baba Askofu Chomba ametoa Rai hiyo Jumamosi iliyopita wakati akizungumza na Mandaitv Online muda mfupi baada ya mchungaji Yonanes Chawinga wa huduma ya God’s Congregation Intimacy Ministry (GCIM), kuwekwa wakfu rasmi kuwa mchungaji wa huduma hiyo na Askofu mkuu Israel Mwaikonge wa huduma ya Calvary Mission Church.
“Natamani wachungaji wasome, elimu bora itazaa wachungaji bora ambao watafundisha watu neno la Mungu ipasavyo.
“Nitoe mwito kwa mchungaji Chawinga na wachungaji wengine watambue kuwa kizazi kimebadilika, kizazi tulichonacho ni kizazi cha kwanini, hivyo wajiendeleze zaidi kielimu,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa jamii haiwezi kutenganisha mambo ya kiroho na ya kimwili na kwamba ni lazima vyote viende pamoja.
Alifafanua kuwa Kristo alikuwa mtu wa maana kubwa hapa duniani, hivyo mchungaji Chawinga aige mfano wake anapotekeleza majukumu yake ya kiroho na kimwili.
Kuhusu jukumu la wake za wachungaji amesema mke afanye kazi inayompasa kwa ajili ya kusapoti huduma ya mumewe, lakini atambue kuwa ni msaidizi na kwamba yeye hajawekwa wakfu kwa huduma hiyo.
“Binafsi mwanamke namwamini katika huduma mbalimbali hivyo anapaswa kujiamini na kujitambua kwa nafasi aliyo nayo,” alisema.
Kwa upande wake Mchungaji Chawinga ambaye pia ana huduma ya Kinabii, akizungumzia suala la elimu amesema moja ya mambo ya msingi anayotarajia kuyafanya ni pamoja na kutangaza neno la Mungu na kujiendeleza kielimu.
Mchungaji Chawinga ambaye kitaaluma ni mwuguzi msaidizi aliyeajiriwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), amesema Askofu Chomba ni mwalimu wake hivyo anazingatia ushauri wake.
Awali Askofu Mwaikonge alisema hatua ya Mchungaji Chawinga kusimikwa ni tukio kubwa kwa kuwa kuitwa na Mungu kwa huduma hiyo ni neema kubwa sana.
