
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amekabidhi vifaa tiba kwa ajili ya huduma za matibabu katika hospitali ya wilaya ya Makete.
Dk. Mollel amekabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kutoka Mfuko wa Doris Mollel wakishirikiana na Segal Family Foundation.
Msaada huo unalenga kuwasaidia watoto njiti wanaozaliwa katika hospitali ya wilaya hiyo. Baada ya kukabidhi msaada huo Dk. Mollel ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel inayoongozwa na Doris Mollel kwa kuendelea kusaidia jamii katika masuala ya uzazi na kutoa mwito kwa Taasisi mbalimbali nchini kuwa Wazalendo na kujitoa kusaidia jamii.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Doris Mollel, alisema Taasisi yake imekuwa ikijishughulisha na kusaidia huduma za uzazi na matunzo ya Watoto Njiti na tayari ameshazunguka maeneo mbali mbali nchini na kufanya kazi na wilaya zaidi ya 45.
Kwa upande wake mbunge wa Makete, Festo Sanga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Makete.
