
Eritrea imeanzisha mashambulizi kwenye mpaka wake na Ethiopia kwa kile kinachoonekana kuwa mwendelezo wa mapigano mapya yalioanzishwa na serikali ya Ethiopia dhidi ya vikosi vya Tigray, wakati viongozi wa Tigray wakishauri watu wake kuwa tayari kwa vita kamili.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP vikosi vya Eritrea vinashirikiana na vile vya Ethiopia pamoja na makundi shirika yenye silaha, kulingana na msemaji wa TPLF Getachew Reda.
Kupitia ujumbe wa twitter, Reda amesema Eritrea inatumia jeshi lake lote pamoja na vikosi vya ziada, wakati vikosi vyake vikiwa imara kulinda maslahi yao.
Mamlaka za Tigray kupitia ujumbe wake jana Jumanne zimeshauri watu wake kuwa tayari kwa vita ambavyo “vitaangamiza kabisa adui zao na kuwapa ushindi wa kudumu.”
Mfanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu kwenye mji wa Kaskazini mwa Ethiopia wa Adigrat ameambia shirika la habari la AP kwamba vikosi vya Eritrea vimeanza kurusha makombora kwenye maeneo jirani.
