Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatatu Septemba 22, 2025, akiwa Tunduru mkoani Ruvuma, amesema kuwa kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita imeunganisha umeme kwenye vijiji vyote vya mkoa huo pamoja na nusu ya vitongoji kote nchini.
Hatua hii imezidi maelekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020, ambayo ilielekeza vijiji vyote viwe vimeunganishwa na umeme kufikia mwaka 2025.
Akizungumzia utekelezaji wa ahadi za Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, hususan kuhusu ujenzi wa kongani za viwanda katika wilaya zote nchini, Dkt. Samia alisema Tunduru pia itajengewa kituo cha kupokea na kupooza umeme wilayani humo, chenye uwezo wa megawati za ziada 116 zitakazotumika kama akiba.
Lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika mkoa huo.
Aidha, Dkt. Samia aliongeza kuwa serikali yake ipo kwenye mchakato wa kufufua viwanda vya kubangua korosho wilayani Tunduru.
Viwanda hivyo vilibinafsishwa na baadaye vikakosa kuendelea na uzalishaji.
Amesema kufufuliwa kwa viwanda hivyo kutahitaji upatikanaji wa umeme wa kutosha, na ndiyo maana amesisitiza kuongeza uzalishaji wa umeme wilayani humo ili kukidhi mahitaji yatakayotokana na ongezeko la viwanda na kongani mpya zitakazojengwa endapo CCM itapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi. PICHA KWA HISANI YA ITV
