
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema Serikali ina wajibu wa kutafuta njia za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali na sio vinginevyo na haitarajiwi kuonwa ikikaa kimya wakati wananchi wanalalamika.
Amesisitiza kuwa Serikali kazi yake ni kuweka mipango ya kutatua changamoto husika na imethibitisha dhamira na jukumu lake la kutekeleza hilo.
Chongolo ametoa kauli hiyo juzi Agosti 2, 2022 alipokuwa akizungumza na wananchi na wanaCCM wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Chekimaji.
“Niwapongeze kwa kupata kituo cha afya kizuri sana na hongereni kwa kuletewa fedha nyingi lakini kubwa niwaletee salamu za Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,wakati namuaga kumueleza nakuja mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kusalimiana na kuwatembelea wana-CCM na wananchi ameniambia niwasilimu sana.
“Niwahakikishie anawapenda sana, changamoto zenu anazijua ikiwamo barabara ya TPC hadi Boma kwa hiyo muwe na uhakika kwamba ataweka msukumo na kuipa kipaumbele kuhakikisha inajengwa. Ndugu zangu nimewapongeza kwa kupata fedha za kituo cha afya lakini niwapongeze zaidi kwa ninyi wenyewe kuchanga zaidi ya Sh. milioni 11
“Kuhakikisha mnaanzisha ujenzi wa zahanati kwasababu mlikuwa mnajua madhila ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma za afya, hongereni sana, lakini niipongeze halmashauri ya wilaya ya Hai kwa kuona jitihada zenu na kuleta Sh.milioni 28 kuongeza nguvu zenu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo tulilosimama hapa la OPD ambalo fedha kwa ajili ya kituo cha afya zililikuta tayari limeshapauliwa, hongereni sana,” amesema Chongolo.
Aidha amewapongeza kwasababu michango waliyotoa ilionesha dhamira yao ya kujikwamua na changamoto ya umbali wa kufuata huduma za afya a hiyo inoanesha ni namna gani walivyowazalendo na wanavyojipenda kujitafutia kwa kutumia nguvu zao na namna ya kusogeza huduma karibu yao.
Amefafanua pale Serikali inapofanya jambo jema la utekelezaji wa Ilani ambayo imewapatia kutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano wananchi hawafanyi chochote cha kuwapongeza hivyo ni lazima jamii ijenge utamaduni wa kupongezana pale inapofanya mambo mazuri au wengine wanapofanya mambo mazuri.
“Tusisubiri kulaumu na kutengenezeana nongwa kwasababu binadamu ana pande zote mbili, kukosea ni sehemu ya maisha lakini kupatia pia si lazima tuwape mkono hongereni sana watumishi wa Serikali kwa kufanikisha hili, mmesema hapa barabara na mimi niwahakikishie barabara hii itajengwa.
