Ndege ya Air India iliyokuwa ikielekea London ikiwa na watu 242 imeanguka dakika chache baada ya kupaa kutoka katika Jiji la Ahmedabad, Magharibi mwa India, tukio lililotokea leo Alhamisi.
Taarifa kutoka kwenye shirika hilo na mamlaka za usalama nchini humo, zimethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hawakueleza kama kuna vifo vilivyothibitishwa.
Air India ilisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick nchini Uingereza, huku maafisa wa polisi wakieleza kuwa ilianguka katika eneo la makazi ya raia karibu na uwanja wa ndege huo.
Chanzo kimoja kililiambia shirika la habari la Reuters kuwa watu 242 waliokuwemo walijumuisha watu wazima 217 na watoto 11. Kati yao, 169 walikuwa raia wa India, 43 Waingereza, saba Wareno, na mmoja alikuwa Mkanada.
Tovuti ya kufuatilia safari za ndege ya Flightradar24 ilisema kuwa ndege hiyo ilikuwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, mojawapo ya ndege za kisasa zaidi za abiria zinazotumika kwa sasa.
Ajali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya ndege kupaa, kulingana na taarifa za televisheni. Kituo kimoja cha televisheni kilionyesha ndege hiyo ikipaa juu ya eneo la makazi, kisha ikatoweka kwenye skrini kabla ya wingu kubwa la moto kupanda juu kutoka upande wa nyuma ya nyumba hizo.
Picha zilizorushwa pia zilionyesha mabaki ya ndege yakiteketea kwa moto, huku moshi mzito mweusi ukipanda angani karibu na uwanja wa ndege.
Pia zilionyesha watu wakibebwa kwa machela na kupelekwa kwa magari ya wagonjwa.
Kulingana na mamlaka ya udhibiti wa safari za anga katika uwanja wa ndege wa Ahmedabad, ndege hiyo iliondoka saa 7:39 mchana (0809 GMT) kutoka barabara ya kurukia ndege ya 23. Ilitoa mwito wa dharura wa “Mayday,” kuashiria hali ya hatari, lakini baadaye hakukuwa na majibu yoyote kutoka kwa ndege hiyo.
See translation
