
Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Boko Haram wamewaua kwa risasi wakulima 11 kusini mashariki mwa Niger, tisa kati yao ni kutoka Niger na wawili kutoka Nigeria.
Meya Issa Bonga, wa mji jirani na mahala shambulio lilipotokea alithibitisha hilo jana Jumatano ambapo ameiambia AFP kwamba “ Wakulima 11 waliuawa kwa kupigwa risasi Jumanne na wapiganaji wa Boko Haram, umbali wa kilomita 7 kutoka mji wa Toummour.
Meya huyo amesema waathirika hao walikuwa wameenda kukata kuni msituni katika mji huo unaopatikana katika jimbo la Diffa karibu na bonde la ziwa Chad eneo muhimu kijeshi, ambako mipaka ya nchi nne ambazo ni Cameroon, Chad, Niger na Nigeria inakutana.
Boko Haram na hasimu wake, kundi la Islamic State in West Africa Province (ISWAP), waliweka ngome zao katika visiwa vingi vidogo katika bonde kubwa la ziwa Chad.
