
YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Kikao cha Baraza la Ushauri mkoa wa Ruvuma, kimeamua kuundwa Tume itakayofuatilia mienendo ya kampuni zinazotekeleza miradi ya umeme vijijini (REA).
Tume hiyo itachunguza kusuasua kwa utekelezaji wa miradi hiyo hali inayoleta kero kwa wananchi katika mkoa huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate, amemwomba mkuu wa mkoa huo na wakandarasi wanaosimamia utekelezaji wa miradi kujiridhisha na sababu inayosababisha kusuasua kwa utekelezaji wake.
Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama, kwa upande wake ametaka kuchukuliwa uamuzi mgumu wa kuwakataa wakandarasi wanaochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Mhagama ametolea mfano wa mkandarasi aliyekuwa anasimamia mradi wa maji jimboni kwake kuwa alichukua uamuzi mgumu wa kumsimamisha.
Juma Pandu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo amekiomba kikao hicho kutafuta mbinu mbadala za kuwafanya wakandarasi hao wafanye kazi haraka badala ya kuvunja mkataba kwa kuwa watawasababishia hasara kubwa.
Mhandisi Stella Manyanya Mbunge wa Nyasa ameshauri kabla ya kuvunja mkataba kikao kinatakiwa kijiridhishe sababu ya wakandarasi wa miradi kusuasua.
