
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, ameitaka Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), kuwashirikisha wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Pia ametoa mwito kwa Jumuia hiyo kujenga utaratibu wa kuendeleza mazungumzo ya mara kwa mara yatakayo wawezesha kuepuka sintofahamu ambayo inaweza kutokea kutokana na ukimya wa muda mrefu.
Balozi Mulamula ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika kikao cha kujadili masuala ya mtangamano pamoja na uamuzi uliofanywa siku za nyuma na vikao vya ngazi ya juu.
Kikao hicho kilichowakutanisha pamoja watendaji wa Jumuia hiyo pamoja na Mabalozi wa nchi hizo walioko nchini, kimefanyika jijini Arusha.
Balozi Mulamula amesema kama Wizara ya Mambo ya Nje watachukulia shughuli za Jumuia na umuhimu wake kwa kuhakikisha mtangamano unakaa vizuri katika uchumi, biashara, siasa na masuala mingine mtambuka, itawezesha jamii kufahamu kinachoendelea katika Jumuia na hivyo kuwa sehemu ya ushirikiano wa kijumuia.
Kwa upande wake Katibu mtendaji wa Jumuia hiyo, Peter Mathuki, amesema kikao hicho kimelenga kuangalia mbiu ambazo zitatumika katika kuimarisha jumuia hiyo kulingana na malengo tofauti yaliyopo katika kuboresha masuala ya kiuchumi na kibiashara.
Naye Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu, akizungumza kwa niaba ya Mabalozi wa Jumuia hiyo, amewataka mabalozi kuunga mkono misingi, kazi na juhudi za jumuia hiyo ili kuhakikisha inakuwa imara kwani ushindi wake ni fahari ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
