*UN yasema hali itakuwa mbaya zaidi mwakani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, ameonya kuwa ulimwengu unakabiliwa na kile alichokiita janga kwa sababu ya ongezeko la ukosefu wa chakula kote duniani.
Guterres amesema vita nchini Ukraine vimechangia hali hiyo iliyotokana na mabadiliko ya tabianchi, janga la virusi vya corona, ukosefu wa usawa na kusababisha mgogoro wa njaa duniani ambao haujawahi kushuhudiwa na ambao tayari unawaathiri mamilioni ya watu.
Katika taarifa kwa njia ya video kwa maofisa mbalimbali kutoka mataifa tajiri ya yanayoinukia kiuchumi wanaokutana mjini Berlin, Guteress amesema kuna hatari kwamba mabaa mengi ya njaa yatatangazwa mwaka huu wa 2022 na huenda mwaka 2023 ukawa mbaya zaidi.
Guteress amesema kuwa mavuno barani Asia, Afrika na Amerika yataathirika wakati wakulima kote ulimwenguni wakijitahidi kukabiliana na ongezeko la bei ya mbolea na nishati.
