
Mkazi wa kijiji cha Lusala, wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, Linus Mtega (52), amefariki dunia baada ya kupigwa na tofali usoni wakati akicheza muziki kwenye sherehe za ujenzi wa makaburi.
Razalus Kufabasi (50), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kusababisha mauaji hayo ya kikatili kwa kile kinachodaiwa kuwa alifanya hivyo baada ya kumfuma akisakata muziki huku akiwa amemkumbatia mke wa mshukiwa huyo.
Akithibisha kutokea kwa tukio hilo kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issa amesema Mtega alichanika kwenye paji lake la uso na kulazimika kukimbizwa kituo cha afya cha Mlangali lakini hakuweza kupona badala yake alifikwa na umauti.
Kamanda Issa amesema baada ya mshukiwa kubaini amesababisha mauaji hayo alijaribu kutoroka lakini alitiwa mbaroni na Polisi kabla ya kufika mbali.
Aidha, Kamanda Issa amelaani tabia hiyo huku akiitaka jamii kuacha wivu uliopitiliza kwani yanapotokea mauaji kama haya familia pamoja na watoto ndio huteseka.
