Skin infected Herpes zoster virus on the arms

Wakati visa vya maambukizi ya Monkeypox vikiendelea kushuka kwenye mataifa ya Ulaya pamoja na Marekani, wataalam wa sayansi wanasema sasa ni wakati wa kuweka kipaumbele cha upatikanaji chanjo ya maradhi hayo barani Afrika.
Mwezi Julai, Shirika la Kimataifa la Afya (WHO), liliorodhesha monkeypox kuwa dharura ya kimataifa, wakati likiomba jumuia ya kimataifa kusaidia mataifa ya kiafrika kuepuka ukosefu wa usawa wa chanjo, kama uliyoshuhudiwa wakati wa janga la Covid-19.
Hata hivyo, macho ya ulimwengu hayakuelekezewa kwenye bara hilo, huku kukikosa taifa hata moja tajiri lililotoa chanjo kwa ajili ya Afrika, wakati wataalam wakionya kwamba hamu ya kusaidia bara hilo huenda ikadidimia kabisa.
Placide Mbala mtafiti wa magonjwa ya virusi kutoka taasisi ya kimatibabu ya Congo amesema hakuna lililobadilika kwa kuwa ulimwengu unashugulikia maambukizi ya monkeypox kwenye mataifa ya magharibi.
Ameongeza kuwa mataifa ya kiafrika ambako ugonjwa huo umekuwa kwa muda mrefu yamekuwa dhaifu ifikapo kwenye masuala ya utafiti, ufuatiliaji, upimaji pamoja na matibabu kwa wagonjwa.
Monkeypox umeambukiza watu kwenye baadhi ya maeneo ya magharibi na kati mwa Afrika tangu miaka ya 70, lakini ulianza kuzungumziwa kwa kina baada ya kuzuka barani Ulaya na Marekani hivi karibuni ambapo wataalam wa afya wamependekeza kwa mara ya kwanza kutumika chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
WHO imesema itaweka mikakati ya ugawaji chanjo ili kuhakikisha mataifa maskini yanazipata pia.
