
Watumishi wa Mungu wamekumbushwa umuhimu wa kuwasaidia wahitaji wanaowazunguka badala ya kujikita kwenye kuwahubiria neno la Mungu pekee.
Nabii Neema Mathew wa Kanisa la Kisima cha Uzima, lililopo Chanika eneo la Zingiziwa, jijini Dar es Salaam, ameyasema hayo wakati wa ibada maalumu aliyoiandaa kwa ajili ya kuwashika mkono yatima, wazee na wajane, Jumapili iliyopita.
Wakati wa ibada hiyo, Nabii Neema, alifanya maombi na kisha kuwagawia fedha wahitaji hao zaidi ya 50 ili kupunguza changamoto za kiuchumi walizonazo sanjari na kula nao chakula maalumu kanisa lake lilichowaandalia.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Nabii Neema amesema ililenga kuonesha upendo kwa wahitaji hao kwa kuwa si vema kuwahubiria neno la Mungu pekee wakati wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa chakula.
Ametanabahisha kuwa kanisa la sasa linatakiwa kutokuwa na ubaguzi wa dini wala dhehebu kwa wahitaji bali liwe na upendo kama Mungu anavyotaka maana hata katika mandiko matakatifu amesema “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi pendaneni vivyo hivyo.
“‘Hivyo, watu wote watatambua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” alilifafanua kwa kunukuu maneno hayo kutoka katika Biblia.
Pia alisema Yak. 1:27 inasema, “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa,” amesema.
Na aliwakumbusha kuwa Yesu alikuja duniani siyo kwa Wakrito bali kwa watu wote, hivyo udini na udhehebu hautawapeleka mbinguni bali kwa kutenda mambo yaliyo mema na kuwapenda wengine. Kwa upande wao wahitaji hao walimshukuru nabii huyo kwa misaada aliyoitoa kwani amefanya jambo jema la kuwakumbuka wao kama wahitaji, kwani vitu alivyovitoa vitawasaidia kupunguza changamoto za kiuchumi walizokuwa nazo.


