
Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (kushoto), akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, David Concar, nyumbani kwa balozi huyo wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa kike, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inalinda haki za mtoto wa kike kielimu, kiuchumi na kijamii.
Waziri Ndalichako amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Balozi wa Uingereza nchini, David Concar, katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.
Amesema Serikali inaendelea kusimamia sheria ambazo zinalenga kuwalinda watoto wa kike hususan kuwapatia elimu ambapo Mwaka 2016 ilifanyia marekebisho sheria ya elimu ili kuendelea kumlinda mtoto wa kike katika kumpatia elimu.
Ameongeza kuwa Serikali imeimarisha suala la unasihi na malezi shuleni pamoja na kuendelea kujenga hosteli kwa ajili ya watoto wa kike ili kuhakikisha hawatembei umbali mrefu kwenda na kurudi shule ili kuwaepusha na changamoto zinazoweza kukatiza masomo yao.
Waziri Ndalichako amesema kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP), Serikali inakusudia kujenga shule 26 maalum kwa ajili ya mtoto wa kike, moja kwa kila mkoa.
Amesema shule hizo ambapo kila moja itachukua wanafunzi 1000 kila, serikali imeshatenga fedha za kuanzia kujenga shule 10.
Ametanabahisha kuwa zote hizo ni juhudi za kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila changamoto lakini pia ushiriki wa mtoto wa kike katika sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake Balozi Concar amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na ushirikiano na Serikali ya Uingereza katika maeneo tofauti hususan ya kumwezesha mtoto wa kike ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametangaza kuongeza msaada wa paundi milioni 55 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya elimu hapa nchini.
