
Mtaalam wa Virutubisho Tiba, Abdallah Mandai, ametoa mwito kwa wanaosumbuka kwa tatizo la mzio (aleji), kutumia mafuta ya nyonyo kuondokana na tatizo hilo.
Ametoa ushauri huo leo Oktoba 15, 2021, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia namna jamii inavyohaingaka kutatua matatizo mbalimbali ya kiafya.
“Daktari Hemant Pathak wa India katika moja ya tafiti zake kuhusu tatizo la mzio, alibaini kuwa mwenye mzio akinywa matone matano ya mafuta ya mbarika (mbono), kwenye glasi moja ya maji ya uvuguvugu yaliyoongezewa kijiko kimoja cha mezani cha asali kila asubuhi kabla ya kula chochote anaweza kujitibu mzio wa ngozi, tumbo na mifereji ya pua,” amesema Mtaalam Mandai.
Mandai, amesema athari zinazoweza kujitokeza kwa mwenye mzio ni pamoja na kuvimba mwili, kupiga chafya, kukohoa, mafua, kujikuna, kupumua kwa taabu, kutapika kuharisha na kunyonyoka nywele.
Pamoja na kutumia mafuta ya nyonyo pia mgonjwa atumie majani ya mwarobaini. “Chukua kilo moja ya majani ya mwarobaini, chemsha kwenye lita tano za maji muda wa dakika 15. Oga mwili mzima yakiwa ya vuguvugu.
“Au chukua nusu kilo ya wali uliopikwa, pondaponda uwe kama uji, ongeza maji lita tano chemsha muda wa dakika 10, oga mwili mzima kwa maji hayo.
“Pia unaweza kutengeneza lita mbili za maji ya majani ya chai, hakikisha unaweka majani mengi, ongeza chumvi halafu oga mwili mzima.
“Au chukua bizari vijiko viwili vya mezani, ongeza katika lita tatu za maji, chemsha muda wa dakika 15, oga mwili mzima kwa maji hayo.
“Waweza pia kuchukua lita tatu za maji, kamulia ndimu sita, ongeza vijiko viwili vya mezani vya chumvi ya mawe, chemsha muda wa dakika tano kisha oga mwili mzima, “amesema Mandai.
Mzio unaweza kutokea baada ya kukutana na vitu kama vumbi, vipodozi, manyoya ya wanyama, chanjo, baridi, vyakula na vinywaji. Kitu kimoja kinaweza kusababisha athari za aina tofauti kwa watu tofauti wenye mzio.
