
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amezindua kile ambacho wengine wanakielezea kuwa ni jaribio kubwa zaidi kuweza kufanyika katika mabadiliko ya kanisa hilo kwa miaka 60.
Miaka miwili ya mchakato wa kupata ushauri kutoka makanisa yote ya kanisa katoliki duniani kuhusu mwelekeo wa kanisa hilo kwa siku zijazo umeanza Vatican mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya waumini wa Katoliki wanamatumaini kuwa mabadiliko yanaweza kugusia mambo kama wanawake kuongoza ibada, mapadre kuoa na uhusiano wa jinsia moja.
Wengine wakihofia mabadiliko hayo yataathiri misimamo ya kanisa hilo.
Wanasema suala la kuzingatia kufanya mageuzi linaweza kuathiri masuala mengine yanayolikabili kanisa kama rushwa na kupungua kwa idadi ya waumini.
Papa Francis amewataka wakatoliki kusikilizana na kuacha kuweka vizuizi.
