Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesaini mkataba mpya wa muda mrefu utakaomuweka katika klabu hiyo kwa kipindi kirefu zaidi. Mkataba wake wa awali, alioutia saini Septemba 2024, ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu ujao.
Arteta, mwenye umri wa miaka 44, ameibadilisha Arsenal tangu alipokabidhiwa timu hiyo, huku msimu uliopita akiiongoza klabu hiyo kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 22, kufuatia kumaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo.
Chini ya Arteta, Arsenal pia ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili katika historia yake, ingawa ilipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Paris Saint-Germain. Kocha huyo pia ameiongoza Arsenal kutwaa FA Cup moja na Community Shield tatu.
Akizungumzia mkataba huo mpya, Arteta amesema ni heshima kubwa kuendelea na safari yake Arsenal, akisisitiza kuwa anafurahia kufanya kazi na watu wenye uwezo na wanaotaka kuona klabu hiyo ikifanikiwa. Amesema uhusiano uliojengwa na klabu pamoja na mashabiki umeleta kumbukumbu za kudumu na kwamba bado wana mengi ya kufanikisha kwa pamoja.
Arteta pia ametoa shukrani kwa Stan Kroenke na Josh Kroenke kwa imani na msaada wao, akisema anajisikia kuheshimiwa kuendelea kuiongoza Arsenal katika kipindi muhimu cha historia yake ya miaka 140. Ameongeza kuwa anaona upendo na heshima kutoka kwa mashabiki na kwamba yeye pamoja na familia yake wanawathamini pia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Richard Garlick, amesema kuendelea kwa Arteta ni hatua muhimu katika historia ya klabu hiyo. Garlick amesema Arsenal inalenga kujenga enzi ya ushindi pamoja na Arteta, akisisitiza kuwa kocha huyo ana imani, dhamira na uelewa wa kile kinachohitajika kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu Emirates.
