
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inakusudia kukamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa Tisa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba wa ujenzi huo, Waziri mwenye dhamana, Dk. Doroth Gwajima, amesema litakuwa na uwezo wa kuchukua watumishi 400 kwa awamu ya kwanza.
Dk. Gwajima amesema Makubaliano baina ya Wizara na Mkandarasi Nandhra, yamekuja mara baada ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa sh. bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la wizara ambalo litajumuisha Idara Kuu ya Afya na Idara Kuu Maendeleo ya Jamii na kwamba ni imani mradi utaanza kwa wakati na kukamilika ndani ya miezi 24 kama ilivyopangwa.
“Hatutegemei kipindi cha miezi 24, kipite kama maelekezo ya Serikali yalivyotaka halafu kazi iwe haijakamilika, ni imani yetu mkandarasi atakuwa na mpango kazi utakao ainisha kila siku nini kitakuwa kinafanyika,” amesema Waziri Dk. Gwajima.
Dk. Gwajima ameitaka Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji ndani ya wizara kutowaachia kazi mkandarasi na kukaa pembeni badala yake waweke kadi ya maendeleo (Score card) ya ujenzi na iwe inakaguliwa kila Jumatatu ili kubaini maendeleo ya ujenzi huo, huku akihimiza viongozi wa wizara kufanyia vikao vyao, eneo la ujenzi (Site meetings).

Kwa upande wao Wakala wa Ujenzi Nchini (TBA), ambaye ni mkandarasi mshauri, amemhakikishia Waziri na ujumbe wake kuwa, Mkandasi huyo, watamsimamia ili kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi kilichopangwa au chini ya hapo, huku akisema ana imani na Mkandarasi Nandhra kutokana uzoefu wake.
Naye Mkandarasi Iqbal Singn, akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Nandhra Engineering and Constructions, amesema wanashukuru kwa kuaminiwa na Serikali lakini wao kama kampuni watahakikisha wanazingatia makubaliano ya mkataba na kukamilisha kazi kwa wakati.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, imesaini mkataba na Mkandarasi Nandhra wa mjini Morogoro, ambapo hafla hiyo imehudhuriwa pia na Makatibu Wakuu wa Wizara, Profesa Abel Makubi wa Afya Kuu na Dk. James Jingu, Katibu Mkuu, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
