
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga limemtia mbaroni Heneriko John (53), kwa tuhuma za kumwua kwa panga mkewe.
Kamanda wa polisi mkoa huo, George Kyando, amesema jana Oktoba 5, 2021 saa 3 asubuhi katika mtaa wa wa Mbulu, kata ya Mhongolo, wilaya ya Kahama ambapo mtuhumiwa alimwua mkewe Regina Jiyenze (45).
Kamanda Kyando amesema mtuhumiwa huyo alimwua mkewe kwa kumkatakata kwa panga kichwani na mabegani, kisha alikwenda kujisalimisha polisi.
Amesema uchunguzi wa awali umeonesha chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa sio mwaminifu kwenye ndoa yao.
Aidha, kamanda huyo amesema mita 20 kutoka eneo la tukio jeshi hilo lilikuta panga lenye damu linalodaiwa kutumiwa na mtuhumiwa huyo wakati akitenda kosa hilo.
“Mtuhumiwa alitumia mbinu ya kumvizia mke wake na kumkata mapanga wakati akiwa nyumbani kwa balozi Manungu Bundala, alipofika kwa ajili ya kushitaki kutishiwa kuuawa na mume wake, ndipo alipokatwa mapanga sehemu za kichwani na mabegani na kufariki dunia,” amesema.
