Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amekagua maendeleo ya miradi ya utalii ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Pugu-Kazimzumbwi, inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), iliyopo Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, leo Oktoba 20, 2026.
Miradi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kwa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), inayowezeshwa kupitia Tozo ya Maendeleo ya Utalii (Tourism Development Levy – TDL), kwa lengo la kuboresha miundombinu na huduma za utalii na kuongeza uwezo wa kupokea wageni.
Katika ziara hiyo, Waziri Kijaji amekagua ujenzi wa cottages na miundombinu saidizi, miundombinu ya burudani pamoja na mabanda ya kupumzikia watalii katika eneo la Bwawa la Minaki na kueleza kuwa mashabiki wa soka ambao hawapendi kelele za uwanjani, watapata fursa za kuangalia AFCON wakiwa kwenye eneo hilo la utalii.
Ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande (Mb), na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, walioshiriki kufuatilia maendeleo ya miradi hiyo.
Uwekezaji huo unalenga kuongeza mvuto wa Hifadhi ya Pugu-Kazimzumbwi kama kivutio cha utalii wa asili, kuboresha uzoefu wa watalii na kuimarisha maandalizi ya kupokea wageni wakati wa AFCON, huku ukichangia kukuza utalii wa ndani na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa.
