
Wanawake zaidi ya 400 katika manispaa ya Shinyanga ni miongoni mwa makundi ya watu waliopata vyandarua siku ya maadhimisho ya siku ya Malaria duniani mwaka huu, 2022.
Vyandarua hivyo vilivyotolewa na Taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Amref, vimegawiwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel kwa kushirikiana na mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Pascal Katambi.
Hafla hiyo imefanyika wakati kilele cha warsha ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Malaria na kuhamasisha umuhimu wa kupata chanjo ya corona.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dk. Mollel ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuja na mkakati huo wa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuweza kutoa misaada mbalimbali inayogusa maisha ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Doris Mollel, amesema lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu ya ugonjwa malaria na namna ya kujikinga pamoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili waweze kujikinga na janga hilo nchini na duniani kote.
“Zoezi limefanyika katika mikoa mitatu kwa kushirikiana na Amref kwa mikoa ya Simiyu, Kagera na Shinyanga na tunaishukuru Serikali kwa kutuwekea mazingira wezeshi sisi taasisi binafsi kuweza kufanya kazi na kutoa mchango wetu ndani ya jamii,” amesema Doris.
