
Wanajeshi wa Israel wamefanya uvamizi katika wilaya ya Jenin iliyoko Ukingo wa Magharibi, ambako wanaishi washambuliaji waliohusika na mkururo wa mashambulizi ya hivi karibuni.
Operesheni hiyo ya kijeshi imefanyika jana Jumapili baada ya mshambuliaji mmoja aliyejihami kwa silaha kufyatua risasi siku ya Alhamis mjini Tel Aviv na kuwaua watu watatu na kujeruhi wengine.
Takriban watu 14 wameuawa katika kipindi cha siku chache zilizopita katika mojawapo ya mlipuko mbaya zaidi wa machafuko dhidi ya Waisraeli.
Shirika la habari la AFP limesema katika kipindi hicho pia, Wapalestina 10 wameuawa, wakiwemo wapiganaji.
Wilaya ya Jenin inachukuliwa kuwa ngome ya wapiganaji wa Palestina. Vikosi vya Israel vimekuwa vikiendesha mashambulizi ndani na nje ya eneo hilo, kujaribu kuzuia kile Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett amekiita wimbi jipya la ugaidi.
