
Mwaka mpya wa masomo nchini Nigeria umeanza mwezi huu wa Septemba lakini zaidi ya shule 600 bado zimefungwa kutokana na visa vya utekaji nyara kutoka kwa makundi yenye silaha nchini humo.
Umoja wa Mataifa unasema Nigeria ina idadi kubwa zaidi ya watoto wasiohudhuria masomo, na kwamba inaendelea kuongezeka.
Kwenye mji mdogo wa Sabo Kusini mwa jimbo la Kaduna kundi la wanafunzi limekusanyika pamoja kutokana na ghasia zinazoendelea.
Wengi wa wanafunzi hao walifika kwenye kambi maalum za hifadhi wakiandamana na wazazi Novemba mwaka jana baada ya kutoroka makwao kutokana na ghasia.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), limesema zaidi ya wanafunzi milioni 20 wa Nigeria hawapo shuleni, likiwa ongezeko la milioni mbili kulinganishwa na utafiti wa Mei mwaka jana.
Hata hivyo, serikali ya Nigeria imekanusha takwimu hizo ikisema kwamba hali imeimarishwa wakati ufadhili wa sekta ya elimu ukiongezwa.
