
Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ameitaka jamii kuwaenzi waalimu kwani wanamchango mkubwa katika malezi ya watoto.
Mama Zainab ameyasema hayo jana kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wanafunzi waliofanya katika shule ya Laureate,iliyoko Chukwani, Wilaya ya Magharibi B, Unguja.
Mama Zainab amekumbusha jukumu la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuwa karibu na shule binafsi ili kuzisaidia kuinua viwango vya ufaulu kwenye mitihani ya taifa.
Kadhalika amewataka wazazi nchini kutoa ushirikiano kwa waalimu katika kuwapatia watoto elimu bora, kuwajenga katika nidhamu, heshima na malezi yaliyotukuka.
“Tutakapokuwa na ushirikiano wa dhati na waalimu, tunachagiza kuwa na taifa lenye vijana waliojengwa kimaadili na kiutawala, sifa ambazo msingi wake hujengwa sasa,” amesema.
Amesema njia mojawapo ya wazazi kuwa karibu ni kujitahidi kulipa ada za watoto wao kwa wakati pamoja na mara kwa mara kufuatilia maendeleo yao shuleni. “Mkiwa wazito kulipa ada mtakwamisha mipango ya shule kuimarisha upatikanaji wa vitabu na kutengeneza miundombinu kwa ajili ya mazingira mazuri ya kufundishia,” amesema.
Katika risala yake, uongozi wa Laureate umesema wingi wa kodi zinazolipwa serikalini ni moja ya mambo yanayozorotesha kasi ya maendeleo ya shule hiyo na umeiomba serikali kufikiria kupunguza ili kuzisaidia shule binafsi kuongeza maslahi ya walimu ambao ni sehemu muhimu ya mafanikio yanayopatikana.
