Bunge limeambiwa kuwa Serikali inafanyia maboresho vitambulisho vya ujasiriamali na ukomo wake utakuwa ni mwaka mmoja tangu siku mhusika anakilipia.
Maboresho hayo ni pamoja na kuweka jina na picha ya mjasiriamali husika katika kitambulisho hicho na kuisha muda kulingana na kalenda ya mwaka.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu, leo bungeni jijini Dodoma, Naibu waziri wa Tamisemi, Dakta Festo Dugange amesema lengo la mabadiliko hayo ni kupunguza usumbufu.
Amefafanua kuwa Machi mwaka 2018, serikali kwa kuthamini na kuwajali wajasiriamali na watoa huduma ndogondogo ilianzisha utaratibu wa vitambulisho hivyo ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na tulivu.
Awali Mbunge Hawa Mchafu alihoji iwapo serikali ina mpango wa kurasimisha vitambulisho vya ujasiriamali.
