
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema ufichuzi wa nakala za ‘Pandora papers’ utaimarisha uwazi wa umiliki fedha unaohitajika nchini Kenya na duniani kwa ujumla.
Ufichuzi mkubwa wa nakala za kifedha uliofanywa na muungano wanahabari wapelelezi ICIJ, unaonesha Rais Kenyatta na familia yake, kisiri walimiliki mtandao wa kampuni zilizofunguliwa katika nchi za kigeni kwa miongo kadhaa.
Kulingana na mwanahabari wa BBC, Ferdinand Omondi, Rais Kenyatta amesema usafirishaji fedha na mapato yaliopatikana kwa njia za uhalifu na ufisadi ulifanyika katika mazingira ya siri na giza.
Rais Kenyatta aliongezea kwamba kitakachofuatia baada ya ufichuzi wa nakala hizo za Pandora na ukaguzi, utaondoa usiri na giza kwa wale ambao hawawezi kuelezea mali na utajiri wao.
Kulingana na ufichuzi huo, uwekezaji uliofanywa katika nchi za kigeni na familia hiyo unashirikisha kampuni moja yenye hisa na dhamana zenye thamani ya $30m, wakfu ambao Rais Kenyatta na mama yake Ngina Kenyatta wameorodheshwa kuwa wamiliki na kampuni moja ya kigeni ambayo haikuweza kugunduliwa wamiliki wake licha ya kwamba ilihusika kununua nyumba moja katikati ya mji wa London ambayo kwa sasa ina thamani ya dola milioni 1.3.
Rais Kenyatta ambaye yuko nje ya nchi ameahidi kutoa taarifa kamili atakaporudi.
