Rais wa Marekani Donald Trump amevituhumu vyombo vya habari vya CNN na The New York Times kwa kueneza taarifa za uongo kuhusu tathmini ya kijasusi iliyoibua mashaka kuhusu mafanikio ya shambulizi la Marekani dhidi ya Iran.
Kupitia chapisho kali aliloliweka kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump amesema vyombo hivyo “vimeshirikiana kudhalilisha moja ya mashambulizi ya kijeshi yaliyofanikiwa zaidi katika historia ya Marekani.”
“Taarifa za uongo CNN, pamoja na New York Times iliyoshindwa, wameshirikiana katika jaribio la kudhalilisha moja kati ya mashambulio ya kijeshi yaliyofanikiwa sana katika historia. maeneo ya nyuklia nchini iran yameangamizwa kabisa! Times and CNN zote zinazomewa na umma!”, ameandika Trump.
Ripoti ya tathmini ya kijasusi iliyovuja hivi karibuni imeeleza kuwa licha ya shambulizi hilo, Iran bado ina uwezo wa kuendelea na mpango wake wa nyuklia. Hata hivyo, utawala wa Trump umekanusha vikali taarifa hiyo, ukisisitiza kuwa mashambulizi hayo yaliteketeza kabisa maeneo yote muhimu ya shughuli za nyuklia za Iran.
Steve Witkoff, mjumbe maalum wa Trump kwa Mashariki ya Kati, ameenda mbali zaidi na kuiita ripoti hiyo kuwa ni “uhaini.” “Ni jambo la kuchukiza, ni uhaini na ni lazima uchunguzi ufanyike. Yeyote anayehusika anapaswa kuwajibika,” amesema Witkoff alipokuwa akihojiwa na Fox News.
Amesisitiza kuwa amesoma tathmini zote za uharibifu na kwamba hakuna shaka kuwa maeneo yote matatu ya nyuklia ya Iran yaliharibiwa kabisa.
