Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mapema Jumapili kwamba jeshi la Marekani limefanya “shambulio lenye mafanikio makubwa” katika maeneo matatu ya vituo vya nyuklia vya Iran, ikiwa ni pamoja na kituo cha kurutubisha uranium cha Fordow.
“Tumekamilisha shambulio letu la mafanikio katika maeneo matatu ya nyuklia nchini Iran… Fordow, Natanz, na Isfahan,” Trump alisema katika chapisho kwenye akaunti yake ya mtandao wa Kijamii.
“Ndege zote sasa ziko nje ya anga ya Iran. Mzigo mzima wa mabomu umerushwa kwenye eneo la, Fordow,” aliongeza.
Tangazo hilo la Trump limekuja siku mbili tu baada ya kusema kuwa ataamua “ndani ya wiki mbili” ikiwa ataungana na mshirika wake Israel kuishambulia Iran.
Shambulio hilo la kushtukiza la Marekani, lililopewa jina la “Operesheni Midnight Hammer,” lilitekelezwa kwa kutumia ndege saba aina ya B-2 ambazo hazikutambuliwa na walinzi wa anga wa Iran, kulingana na Washington.
