
Watu wapatao milioni 7.8 nchini Sudan Kusini ambao ni sawa na theluthi mbili ya watu wote, wanaweza kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika msimu wa mwaka ujao wa Aprili hadi Julai kutokana na mafuriko, ukame na migogoro.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Chakula na Kilimo, la Kuhudumia Watoto UNICEF na la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) yamesema jana Alhamis kuwa uhaba huo ni mbaya zaidi kuliko kilele cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2013 na 2016.
Mashirika hayo yamesema kupungua kwa usalama wa chakula na kuenea kwa utapiamlo kunahusishwa na mchanganyiko wa migogoro, hali mbaya ya uchumi, hali mbaya ya hewa, na kuongezeka sana kwa gharama za chakula na mafuta.
Wakati huo huo, kumekuwa na kupungua kwa ufadhili wa programu za kibinadamu licha ya kuongezeka kwa mahitaji hayo ya kibinadamu.
Ongezeko la bei za vyakula duniani lililochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, muuzaji mkubwa wa nafaka nje, kumeacha mashirika ya kibinadamu na upungufu wa fedha za wahisani.
