
Kamanda wa Taliban na kiongozi wa juu wa mtandao wa wanamgambo wa Haqqani, Anas Haqqani amekutana na Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai kwa mazungumzo.
Ofisa wa kundi la Taliban amesema leo kuwa mkutano huo umefanyika, huku kukiwa na juhudi za Taliban kuunda serikali.
Ofisa huyo wa Taliban ambaye hakutaka kutajwa jina amesema Karzai aliongozana na mjumbe mkuu wa amani katika serikali iliyopita, Abdullah Abdullah, katika mkutano huo.
Mtandao wa Haqqani ni kundi muhimu la Taliban, ambao siku ya Jumapili uliudhibiti mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema nchi yake itafanya kila iwezalo kuepusha migogoro nchini Afghanistan.
Akihutubia leo bunge la Uingereza, Johnson ameielezea hali ya Taliban kuidhibiti Afghanistan kuwa inayoenda kwa kasi kuliko ilivyotarajiwa.

