
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amefanya uhamisho wa baadhi ya maofisa wa Jeshi hilo lengo likiwa ni kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu ya Polisi Dodoma, SACP David Misime, imesema waliohamishwa ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mkonda aliyekuwa Kamanda wa Polisi Tarime Rorya anakwenda kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO).
Mkonda anachukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdi Isango ambaye anakwenda kuwa Mkuu wa Operesheni, mkoa wa Mbeya.
Misime amesema katika mabadiliko hayo yaliyafanyika mapema mwezi huu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zuberi Mwombeji amliyekuwa mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam anakwenda Makao Makuu ya Polisi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Uchumi, na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Kennedy Mgani ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni, mkoa wa Mbeya.
Aidha IGP Sirro amemuhamisha Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Pipi Kayumba kwenda Singida kuwa ofisa mnadhimu namba moja na nafasi yake inachukuliwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Tarcis Idelfonce ambaye alikuwa mkuu wa Polisi wilaya ya Dodoma.
Pia amemhamisha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Jumanne Juke aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Geita kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Kipolisi Rufiji kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ame Anoqie ambaye amehamishiwa Tarime Rorya kuwa ofisa Mnadhimu namba Moja kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Geofrey Sarakikya ambaye anakuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya.
