
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, amepongeza mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akiielezea kuwa inazingatia masuala ya usawa wa kijinsia hali itakayoboresha maendeleo kwa haraka.
Liundi ameyasema hayo jana Jumatatu Juni 28,2021 wakati akizungumzia Siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga (Kiloleli – Kishapu) na Dar es Salaam (Mabwepande, Saranga, Kivule na Majohe) yanayofanyika katika ukumbi wa TGNP Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa TGNP amesema katika siku 100, Serikali ya awamu ya Sita imeonesha mwelekeo mzuri katika kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia.
Amesema kiongozi wa nchi anapozungumza wazi wazi kwamba kwenye masuala ya uongozi atatoa kipaumbele pia kwa wanawake wenye uwezo anaonesha mwanga wa maendeleo.
Amebainisha kuwa wananchi wanaona anachofanya ambapo kwa upande wa Makatibu Tawala ameteua wanawake asilimia 48, hii inakuwa ni kwa mara ya kwanza jamba ambalo ni la kujivunia.
Liundi amesema kutokana na hali hiyo hivi sasa mwendo uliopo ni wa tofauti, mambo yanaenda vizuri kinachotakiwa ni kutoa ushirikiano, wale waliochaguliwa na kuteuliwa waendelee kujitoa, wafanye kazi vizuri kwa uaminifu na uadilifu ili kuonesha kwa vitendo kuwa wanawake wana uwezo wa ziada.
Kuhusu mageuzi ya kilimo ambapo mkulima mdogo, mwanamke ndiyo amebeba taifa katika uhakika wa chakula, Liundi ameshauri mwanamke asije akatupwa pembeni kuwe na mikakati mahsusi ili kuhakikisha kuna ushiriki wa wakulima wadogo wadogo hususan wanawake waliopo kwenye maeneo ya pembezoni.
