
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kutumia vema msamaha uliotolewa na Serikali kusalimisha silaha haramu kwa hiari.
Amesema kipindi cha miezi miwili kilichotolewa na Serikali kitumike lkuzisalimisha kwenye vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, ofisi za watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji.
Sagini ameyasema hayo jna Septemba 5, 2022 jijini Dodoma wakati akizindua Kampeni maalumu ya Usalimishaji silaha inayolenga kuhamasisha wananachi kusalimisha silaha wanazomiliki isivyo halali kwa hiari katika kipindi cha miezi miwili ikiwa na kauli mbiu “Silaha haramu sasa basi, salimisha kwa hiari”.
Sagini amesema uzagaaji silaha haramu umekuwa chanzo cha vifo vya watu katika maeneo mbalimbali kutokana na wamiliki wake kuzitumia vibaya ikiwamo kwa kutokujua misingi na matumizi yake.
Aidha, ameongeza katika kipindi hicho cha msamaha hakuna msalimishaji atakayechukuliwa hatua wala kukamatwa kwa kuwa jambo hilo lipo kisheria na Serikali imeridhia ili kukusanya silaha ambazo zipo katika jamii kinyume cha sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amesema Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa yenye lengo la kuzuia uzagaaji silaha ndogondogo na nyepesi ambapo kila mwaka imekuwa na utaratibu wa kutangaza msamaha kwa watu wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria.
IGP Wambura amesema baada ya silaha hizo kukusanywa zitateketezwa bila kificho mwezi Novemba mwaka huu ili jamii ione na kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine katika udhibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi.
Naye Mwakilishi wa Kituo cha kikanda cha kuzuia na kudhibiti silaha ndogondogo na nyepesi kwa nchi za maziwa makuu na pembe ya Africa (RECSA) Dk. Philip Ouma ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kutekeleza maazimio ya RECSA katika udhibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi ambapo mafanikio yake ni pamoja na nchi za ukanda wa maziwa makuu na pembe ya Afrika kuendelea kuwa salama.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Viongzoi mbalimbali wa Serikali, Asasi za kirai, Viongozi wa dini, Polisi Kata, watendaji wa mitaa, wenyeviti wa Serikali za mitaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.
