
Viongozi wa Jumuia ya maedeleo ya Kusini mwa Afrika, (SADC) wamekubali kupeleka wanajeshi kusaidia kudhibiti uasi unaofanywa na kikundi cha wanamgambo wa Kiislam kinachofanya mauaji na kusababisha taharuki Kaskazini mwa Msumbiji kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
Akihutubia katika mkutano Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, amesema anatambua na kuridhia mshikamano na msaada wa nchi wanachama wa SADC na nchi rafiki ambao wanaunga juhudi kuzuia ugaidi kupata sehemu mwafaka kuendesha mashambulizi katika nchi yake na kanda nzima.
Waraka uliopatikana kwa siri mapema mwaka 2021 ulikuwa unapendekeza kupelekwa takriban wanajeshi 3,000 katika mkoa wa Cabo Delgado, ambapo waasi wameviteka vijiji na miji kadhaa, na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Ghasia zimeongezeka katika sehemu ya Kaskazini mwa Msumbiji yenye utajiri wa gesi uliopatikana mwishoni mwa 2017 na kuna wasiwasi zinaweza kuenea katika nchi jirani.
Hapo Machi 24, wanamgambo wenye uhusiano na kikundi cha Islamic State walianzisha mashambulizi mbalimbali yaliyopangwa kufanyika wakati mmoja katika mji wa Kaskazini wa Palma, ikiharibu majengo na kuua wakazi huku maelfu yao wakikimbilia msituni.
Mashambulizi yamefikia kuongezeka kwa uvunjifu wa amani na kusababisha watu takriban watu 800,000 kukimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 2,800 – nusu yao ni raia.
Viongozi wa Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe walihudhuria mazungumzo jana mjini Maputo.
