KILICHOHARIBU SHOW YA ZUCHU KENYA
Mjadala umeibuka kuhusu changamoto za sauti kwenye show za muziki kwenye mashindano ya CHAN yaliyomalizika, baada ya Rayvanny na Zuchu kulalamikiwa kwa kutofikia viwango vya kimataifa.
Mtangazaji wa Bongo FM, Hajathecredible aliandika kuwa “Technical team ya CHAN kwenye music performance wanapaswa kutuomba radhi… Rayvanny alianza, jana Zuchu pia. Hii haiendani na viwango vya Tanzania.”
Alihoji kwa nini mara zote sauti inakuwa changamoto, akisisitiza kuwa Tanzania ipo kwenye ushindani wa kimataifa, hivyo maonyesho yake lazima yawe na ubora unaokaribiana na wakubwa kama Kendrick Lamar au Tems.
Hata hivyo, meneja wa Zuchu, Kim Kayndo, amewatetea wasanii, akisema tatizo si CHAN wala ubora wa wasanii, bali ni miundombinu ya viwanja vya mpira ambavyo havijajengwa kwa ajili ya live music production ya viwango vya dunia. Amesema viwanja hivyo havina acoustic design, hazina line array na delay speakers za kutosha kuondoa mwangwi.
Amefafanua kuwa kwenye maonyesho makubwa ya kimataifa kama Super Bowl halftime show au FIFA Club World Cup performances, mara nyingi playback hutumika kulinda ubora wa matangazo ya televisheni. “Hii inafanywa ili show iwafikie mamilioni ya watazamaji duniani kwa ubora wa hali ya juu,” amesema.
Kayndo ameongeza kuwa msanii anayepiga live kavukavu kwenye viwanja vya mpira analazimika kuwa na utaalamu wa hali ya juu ili kuendesha sauti sambamba na beat bila kupotezwa na delay na mwangwi.
Hivyo, changamoto inayowakumba wasanii wa Tanzania si uzembe wala hujuma, bali mazingira yasiyo rafiki kwa muziki wa kiwango cha juu.
Kwa mtazamo wake, suluhisho pekee ni kuwekeza kwenye sound infrastructure ya viwanja ili matamasha ya muziki Tanzania yaakisi ukubwa wa wasanii wake kwenye jukwaa la kimataifa.
