
Serikali ya Zambia imetoa rasmi ratiba ya mazishi ya Rupiah Banda aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa nchi hiyo, yatafanyika Ijumaa Machi 18, 2022.
Banda alifariki dunia Ijumaa iliyopita kwa maradhi ya saratani, akiwa na umri wa miaka 85. Serikali ya nchi hiyo imetangaza maombolezi ya siku saba tangu Jumapili.
Kaimu Katibu wa Baraza la Mawaziri la Zambia, Patrick Kangwa, amesema rais huyo wa zamani atazikwa siku hiyo katika Bustani ya Ubalozi, kwenye makaburi ya marais huko Lusaka, Mji Mkuu wa Zambia.
Ameongeza kuwa mpango huo uliwekwa baada ya kushauriana na familia yake.
Kangwa amesema kwenye taarifa kuwa mazishi hayo yatatanguliwa na mazishi ya kitaifa ambayo yatafanywa Machi 17 – Alhamisi wiki hii, ambapo viongozi wa nchi mbalimbali wamealikwa.
Banda alikuwa Rais wa Zambia kuanzia Mwaka 2008 hadi Mwaka 2011.
Yeye amekuwa rais wa tano wa Zambia kufariki tangu Zambia ijipatie uhuru kutoka kwa Uingereza Mwaka 1964.
Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda alifariki dunia mwaka jana.
