Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ameondoka katika kambi ya timu hiyo baada ya kocha Jorge Jesus kusema kuwa hatakuwa katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo dhidi ya Denmark.
Jorge Jesus amesema hana tatizo lolote na Ronaldo na kwamba tayari alizungumza naye kuhusu uamuzi wa kutomuanza katika michezo dhidi ya Norway na Denmark. Kocha huyo amesema ikiwa kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, Gonçalo Ramos ndiye anatarajiwa kuanza katika nafasi ya mshambuliaji.
Baada ya kauli hiyo, Ronaldo aliamua kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa na hakushiriki katika mazoezi yaliyofuata. Taarifa zinaeleza kuwa ndege yake binafsi ilifika Denmark kwa ajili ya kumchukua na kumrejesha Madrid pamoja na familia yake, kabla ya kurejea Saudi Arabia.
Ronaldo amesema baadaye atawaeleza Wazreno ukweli kuhusu sababu zilizomsukuma kuondoka kwenye timu ya taifa, akisisitiza kuwa amekuwa akijitolea kwa taifa hilo kwa muda mrefu na kwamba tayari alizungumza na Rais wa Shirikisho la Soka la Ureno kuhusu suala hilo.
“Nitawaambia ukweli hivi karibuni,” Ronaldo amesema, akieleza kuwa wakati ukifika ataweka wazi sababu zilizomfanya kuchukua uamuzi huo.
Wakati huohuo, dada yake Ronaldo, Elma Aveiro, amemtetea ndugu yake kupitia ujumbe aliouchapisha, akidai kuwa Ronaldo alistahili kuheshimiwa zaidi na kwamba timu ya taifa ilihitaji muundo bora zaidi.
Ameikosoa pia baadhi ya vyombo vya habari vya Ureno kwa kile alichodai kuwa ni kutoa taarifa zenye hisia na makisio.
Kuondoka kwa Ronaldo katika kambi ya Ureno kumeibua mjadala mkubwa, hasa kutokana na kutokea mara tu baada ya kauli ya Jorge Jesus kuhusu kutomuanza katika mchezo huo. Hata hivyo, sababu kamili ya uamuzi wake bado haijawekwa wazi, huku Ronaldo akiahidi kueleza ukweli kuhusu suala hilo baadaye.
