Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimesema hatua zilizochukuliwa na viongozi wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) cha kuwataka mawakili wa kujitegemea kutoshiriki kwenye shughuli za utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ni kinyume cha sheria za nchi na miiko ya kazi za wanasheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Wakili Addo November, amesema TLS, kama taasisi ya kisheria, ina wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha kwamba maamuzi yake hayapingani na sheria iliyoianzisha (TLS Act) na sheria nyingine husika kama Legal Aid Act.
“Maazimio ya TLS yanayolenga kuzuia mawakili wasitoe msaada wa kisheria kwa wananchi ni kinyume na wajibu wa msingi wa wakili kama afisa wa mahakama, na kufanya hivyo ni kuzuia haki kwa wananchi wanyonge. Utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ni wajibu wa kisheria, si hiari, kwa mujibu wa Legal Aid Act [Cap. 21 R.E. 2019],” amesisitiza Wakili November.
Vilevile, amesema taasisi zote za kitaaluma zinapaswa kushirikiana kwa weledi katika kulinda misingi ya haki, usawa, na utawala wa sheria, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuzorotesha huduma za kisheria kwa wananchi wa kawaida nchini.
Nao baadhi ya Mawakili wa Kujitegemea, akiwemo aliyewahi kuwa Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Francis Stolla, wamesema TLS inapaswa kutetea haki za wanachama wake wanaoingia kwenye migogoro na vyombo vingine vya kisheria, pasi na kuvunja sheria na katiba ya nchi.
“Ukisema kwamba wakili asiende mahakamani kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ni ukiukwaji wa maadili ya kazi ya wanasheria. Kwa madai hiyo, chama kinakuwa kimetoa amri kwa wanasheria waende wakakiuke haki au wajibu uliowekwa na sheria,” amesema Wakili Francis.
Wakili Francis ameongeza kuwa iwapo azimio hilo la TLS litatekelezwa, mawakili watakuwa wameingizwa kwenye migogoro ambayo hautaleta tija. Hivyo, akasema ni vyema TLS itumie weledi na busara katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakuta wanachama wake wanapokuwa kwenye majukumu yao, badala ya kuhamasisha mgomo.
