Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili nchini Msumbiji, tarehe 24 Juni 2025, kutokana na mwaliko maalum wa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, kushiriki kama Mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji.
Sherehe hizo za kihistoria zinafanyika leo katika Uwanja wa Machava, uliopo jijini Maputo, na zinahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, huku Tanzania ikiwakilishwa kwa heshima ya juu kupitia kiongozi wake mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais, mwaliko huo maalum ni ishara ya kuimarika kwa Diplomasia ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia, na pia ni uthibitisho wa hadhi na heshima ambayo taifa limejenga kimataifa kupitia ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa na mataifa jirani na duniani kote.
Tukio hilo linaweka rekodi ya kidiplomasia kwa Tanzania, kwani mara nyingi viongozi wa mataifa hushiriki kama wageni wa heshima, lakini si kawaida kwa Rais wa nchi nyingine kupewa nafasi ya mgeni rasmi katika tukio la kitaifa kama la Uhuru wa nchi nyingine- ishara ya heshima ya kipekee kwa Tanzania na uongozi wa Rais Samia.
Msumbiji na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa kihistoria tangu enzi za ukombozi, ambapo Tanzania ilikuwa nguzo muhimu ya kuunga mkono harakati za FRELIMO hadi kupatikana kwa Uhuru mwaka 1975. Hivyo mwaliko huu pia unatafsirika kama kurudisha heshima kwa mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
