Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ataendeleza juhudi za kuufungua Mkoa wa Kigoma kiuchumi kupitia mradi wa kitaifa wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Uvinza.
Akihutubia wananchi wa Kazuramimba, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma leo Jumamosi, Septemba 13, 2025, Dkt. Samia alisema mradi huo wa SGR ni nguzo muhimu ya kukuza biashara na uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla, akiwataka wananchi kutumia vyema fursa zitakazotokana na uwepo wa reli hiyo.
“Kigoma hii ni fursa kubwa sana na hapa Uvinza kutakuwa na kituo kikubwa cha reli hii. Hii ni nafasi ya kipekee kwa wananchi wa Uvinza kuitumia kibiashara kwani itaifungua wilaya hii kwa kiwango kikubwa na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema Dkt. Samia.
Mbali na reli, Dkt. Samia ameahidi kuendelea kutekeleza miradi mingine ya miundombinu mkoani humo, ikiwemo kivuko cha MV Ilagala katika Mto Malagarasi na ujenzi wa barabara za wilaya, hatua aliyoeleza kuwa itasaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.
