Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameonesha huzuni kubwa kufuatia kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Yustino Ndugai.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo, akitoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), watumishi wa Bunge, Wabunge wote aliowahi kufanya nao kazi, pamoja na wananchi wa Jimbo la Kongwa.
“Ninatoa pole kwa familia, wanachama wote wa CCM, watumishi wa Bunge na Wabunge wote aliotumikia nao akiwa Spika, wananchi wa Kongwa, ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Rais Samia.
Aidha, amewaomba Watanzania kuungana pamoja katika kumuombea marehemu apumzike kwa amani na kuwaombea wafiwa wawe na moyo wa subira, faraja na ibada katika kipindi hiki kigumu.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina,” amesema Rais Samia.
Job Ndugai alihudumu kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi 2022.
