
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amepoingeza Serikali kwa kufanikisha maonesho ya Kwanza ya Kanda ya Jumuia ya Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Arusha, kati ya Oktoba 9 na 11, mwaka huu.
Maonesho hayo yaliyohimishwa jana Oktoba 11, 2021, yalilenga kutangaza vivutio na fursa mbalimbali za utalii ndani ya jumuia hiyo.
Mbali ya Dk. Mwinyi, maonesho hayo yalihudhuriwa pia na baadhi ya Mawaziri wa Utalii wa Jumuia hiyo.
“Nawapongeza kwa kufanikisha maonesho haya, ni imani yangu kuwa kupitia maonesho haya nchi zetu za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kujadili njia za kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki. “Natoa mwito kupitia maonesho haya ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa kila nchi mwanachama……..jitihada zaidi zinahitajika katika kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuboresha sera zetu za utalii,” amesema Dk. Mwinyi.
Aidha, Dk. Mwinyi ameitaka Kamati Maalumu ya Kikanda ya Jumuia hiyo kufanya ziara Zanzibar ili kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii pamoja na zile za biashara na uwekezaji.
